![](http://eatv.tv/sites/default/files/styles/detailpageimg/public/news/2025/02/06/EouL7Aw9xDRKsaP3ZbIrz2HdVIOUaD0VIOCXVNlI.jpg?itok=Cy0pYN0l×tamp=1738859483)
Taarifa ya USAID inasema agizo hilo litaathiri wafanyakazi wa kuajiriwa moja kwa moja isipokuwa wale walio kwenye kazi muhimu, uongozi na programu maalumu japo haijulikani ni kazi zipi hasa zimeathirika.
Taarifa hiyo iliyotumwa kwenye tovuti ya shirika hilo, inasema wafanyakazi wamejulishwa kufikia Alhamisi mchana.
Utawala wa Trump umesema USAID inafuja pesa na inahitaji kuundwa ili kuendana na vipaumbele vya sera za rais.
Wafanyakazi wa shirika hilo, wakiungwa mkono na wabunge wa chama cha Democratic, wameandamana kupinga kuondolewa kazini, wakisema hilo litaweka maisha hatarini na kutatiza usalama wa taifa.
Katika taarifa kwenye tovuti yake siku ya Jumanne, USAID inasema itashirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kupanga na kulipia usafiri wa kurejea kwa wafanyakazi waliotumwa nje ya Marekani ndani ya siku 30.
Shirika hilo linalotoa misaada ya kibinadamu kwa zaidi ya nchi 100, limeajiri watu 10,000 duniani kote. Theluthi mbili ya watu hao wanafanya kazi nje ya nchi, kulingana na Congress.
USAID, iliyoanzishwa mwaka 1961, ina bajeti ya karibu dola bilioni 40 kwa mwaka, kiasi cha takriban 0.6% ya matumizi ya serikali, kulingana na takwimu rasmi.