Jumatatu , 16th Mei , 2016

Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda nchini Tanzania (TIRDO) limesema kuwa wafanyabiashara nchini Tanzania ili waweze kufikia viwango vya Kimataifa ni lazima wazingatie ubora wa bidhaa wanazozalisha na wawe na bar-code.

Akiongea wakati akifungua mkutano ulioandaliwa na GS-one na kuwakutanisha wadau na wafanyabiashara wa bidhaa za kuoka nchini Tanzania Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO Prf Mkumbukwa Mtambo amesema kuwa kwa kuzingatia ubora na bar-code bidhaa za kitanzania zitaweza kupata wateja wa ndani na nje ya Tanzania na hivyo watanzania wataweza kukuza biashara zao kimataifa.

Aidha amewataka wafanyabiashara ya bidhaa za kuoka wazingatie ushauri unaotolewa na TIRDO kwani biashara ya chakula ni lazima izingatie viwango na ubora kwani kufanya kinyume chake kunaweza kupelekea matatizo mengi ya kiafya kwenye jamii.

Kwa upande wake Meneja mauzo na Masoko wa kampuni ya GS-one nchini Tanzania Osca Ruhasha amesema kuwa hapo awali wafanyabiashara walipata usumbufu wa kutafuta bar-code tangu nchini Kenya na Afrika Kusini lakini kwa hivi sasa bar-code zinapatikana nchini hivyo wafanyabiashara wachangamkie fursa hiyo ili kuongeza ubora wa bidhaa zao.

Kwa upande wake Mfanyabiashara wa Mikate Bi. Mariam Lyimo amesema kuwa hapo awali alivyokuwa hana bar-code biashara yake ilikuwa ni ya kusuasua ukilinganisha na hivi sasa ambapo wateja wake wanaonekana kuwa na imani kubwa ya bidhaa wanayoitumia hali inayopelekea biashara yake kukua zaidi.