Jumatano , 29th Jun , 2016

Wadau wa kupambana na maambukizi mapya ya Ukimwi mkoa wa Njombe wamesema kuwa kunachangamoto ya baadhi ya watu kutoroka kupata dawa katika vituo vya kuchukulia dawa za kupunguza makali ya Virusi vya Ukimwi.

Mwenyekiti Mtendaji wa Tacaids, Dokta Fatma Mrisho.

Imedaiwa kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakitoroka kutoka katika vituo vya kuchukulia dawa za kupunguza makali ya Virusi vya Ukimwi kwa kushawishiwa na baadhi ya viongozi wa dini kuwa watawaombea na kupona hivyo waache kuzitumia dawa hizo.

Hayo yamebainika katika mkutano wa wadau wa kupambana na virusi vya ukimwi mkoa wa Njombe unaojumuisha viongozi wa dini na waratibu wa Ukimwi mkoani humo.

Mmoja wa wadau hao kutoka taasisi za kidini Mchungaji Elias Msemwa, amesema kuwa kuna baadhi ya waumini wamekuwa wakikimbia dawa na kwenda kwa baadhi wa viongozi wa dini kuombewa ambapo baada ya kuacha dawa hizo asilimia kubwa ya hao hupotelea huko huko.

Hata hivyo Mratibu wa Ukimwi halmashauri ya Mji wa Njombe (Chac), Daniel Mwasongwe, amekiri kuwa katika halmashauri yake kuna watu ambao wanakimbia katika vituo vya kuchukulia dawa na haijulikani kama wamefariki ama bado wanaishi.