Jumamosi , 17th Aug , 2024

Mapigano ya ngumi yalizuka katika bunge la Uturuki siku ya Ijumaa wakati Naibu kiongozi wa upinzani aliposhambuliwa baada ya kumzungumzia mwanasiasa mmoja  wa upinzani  aliyefungwa jela kwa madai ya kuandaa maandamano ya kuipinga serikali.

"Hatushangai kwamba unamwita Can Atalay gaidi, kama vile unavyofanya kila mtu ambaye hayuko upande wako," Sik aliwaambia wabunge wa chama tawala cha AKP katika hotuba.

"Lakini magaidi wakubwa ni wale walioketi katika viti hivi (vya bunge)," aliongeza na kuzua utata.

Picha zilionyesha wabunge wa chama tawala cha Haki na Maendeleo (AKP) wakikimbilia kumpiga ngumi Ahmet Sik, mwanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Uturuki (TIP)  na wengine kadhaa wakijiunga na kumtwanga ngumi, huku wengine wakijaribu kuwashikilia wengine. Damu iliruka na kumwagika kwenye  jukwaa la spika.

Can Atalay alihukumiwa kifungo cha miaka 18 mwaka 2022 baada ya kutuhumiwa kujaribu kuipindua serikali kwa madai ya kuandaa maandamano ya Gezi Park mwaka 2013 ambapo anakana mashatka hayo.

Naibu spika wa bunge alitangaza mapumziko ya dakika 45 baada ya pambano la ngumi.