Rais wa umoja wa mabunge ya nchi za Jumuiya ya Madola kanda ya Afrika, Mh Anna Makinda
Wajumbe wa umoja wa mabunge ya nchi za Jumuiya ya Madola kanda ya Afrika wanakutana Arusha kwa siku Tano kujadili changamoto mbalimbali zinazozikabili nchi za Jumuiya hiyo ikiwemo ya wananchi wa nchi hizo kuendelea kukabiliwa na umaskini wakati uchumi ukionekana kukua.
Rais wa umoja huo kanda ya Afrika ambaye pia ni spika wa bunge la Tanzania Mh. Anne Makinda, amesema mkutano huo wa 45 wa umoja huo unatarajiwa kufunguliwa rasmi na Rais Jakaya kikwete siku ya Alhamisi katika ukumbi wa kimataifa wa AICC na utahudhuriwa na zaidi ya washiriki 500 kutoka nchi hizo.
Mh Makinda ambaye baada ya mkutano huo atakabidhi wadhifa wa uenyekiti kwa spika wa bunge la Lesotho, amefafanua kuwa pia wajumbe hao watajadili tatizo kubwa linalozikabili nchi hizo la kukithiri kwa vurugu na migogoro ya kisiasa hasa wakati wa uchaguzi, ukiukwaji wa haki za binadamu unaowaathiri zaidi wanawake na watoto.
Kwa mujibu wa Mh Makinda amesema wajumbe wa mkutano huo wenye kaulimbiu ya UMUHIMU WA JUMUIYA YA MADOLA KATIKA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA MAENDELEO YA KIUCHUMI NA KIJAMII, watabariki kuanza kwa ujenzi wa jengo la ofisi na kitega uchumi cha umoja huo, linalotarajiwa kujengwa katika mji wa kigamboni jijini Dares salam.
Naye makamu mwenyekiti wa umoja wa wanawake wa nchi za Jumuiya ya Madola Mh Beatrice Shelukindo ambaye ni miongoni mwa watanzania wanaotarajiwa kuwasilisha mada katika mkutano huo amesema suala la usawa wa kijinsia pia litajadiliwa kwa kina katika mkutano huo.
Mwenyekiti msaidizi wa kamati ya maandalizi ya mkutano huo Bw Elisa Mbise amesema maadalizi yote yamekamilika na wajumbe wakiwemo maspika wa mabunge hayo wameanza kuwasili nchini