Jumamosi , 21st Sep , 2024

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewataka vijana nchini kushikamana na kudumisha amani iliyopo ilim kuweza kuwa na Taifa imara.

Dkt. Doto Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Dkt. Biteko amesema hayo Jijini Dar es Salaam wakati akimwakilisha Rais,  Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua Kongamano la Kitaifa la Ajenda ya Amani na Usalama kwa Vijana.
‘’ Wito wangu kwenu shikamaneni shikamaneni shikamaneni! kwa ajili ya kulinda amani ya nchi yetu ili tuwe na Taifa la utulivu na tufurahie maisha yetu, ni vizuri mkakumbuka kuwa hiki ni kipindi cha kujiandaa kuwa baba bora au mke mwema ili baadae kuwa na Taifa bora,’’ amesisitiza Dkt. Biteko.

Akizungumzia maendeleo ya utandawazi na mapinduzi makubwa ya kidijitali ambayo yamekuwa yakitoa fursa lukuki kwa Vijana, Dkt. Biteko  amewaasa vijana kuwa kuwa na matumizi sahihi teknolojia ili iwavushe kimaisha 
"Napenda kuwaasa kwamba matumizi ya teknolojia yakawe na malengo ya kuzalisha na kujitengenezea kipato endelevu, kwa kufanya hivyo kutakuza uchumi na kuonyesha tija ya nguvu kazi yetu katika Taifa letu. Aidha, siyo teknolojia hii inavyotumika sasa kama majukwaa ya uhalifu, uchochezi, udhalilishaji wa kijinsia na uvunjaji wa amani iliyojengwa na vizazi vya Watanzania wengi. Natamani Baada ya Kongamano hili nyie wote mlioudhuria hapa mkawe chachu kwa vijana wenzenu mtakao kutana nao, mkawe dira na walimu bora wa amani,’’amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza  kuwa katika kuhakikisha  kunakuwepo na mazingira mazuri ya ushiriki na ushikikishwaji wa vijana katika masuala mbalimbali ya maendeleo  Serikali imefanyia maboresho Sera ya zamani Maendeleo ya Vijana na tarehe 12 Agosti 2014 Sera Mpya ya Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2007, tolea la mwaka 2024 ilizinduliwa.
‘’Sera hii imeeleza nia ya dhati ya Serikali kuhakikisha vijana wanaandaliwa kuwa wazalendo, waadilifu na wanaoshiriki kudumisha amani na usalama wa nchi yetu. Hii yote ni kutambua umuhimu na nguvu waliyonayo vijana na umuhimu wa ushirikishwaji wao katika katika kujenga nchi yetu. Katika kipindi hiki ambacho nchi yetu ipo katika mchakato wa kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ninawasihi kuwa tumieni fursa hii kuhakikisha mnatoa maoni yenu ambayo pamoja na mambo mengine yatawezesha ushirikishwaji wa vijana kwenye kwenye maendeleo, lakini hasa katika misingi ya amani na usalama na mtumie ubunifu wenu kupendekeza mikakati rafiki kwa vijana itakayowawezesha kushiriki kujenga aina ya Tanzania tuitakayo miaka 25 ijayo. ’’ Amesisitiza Dkt. Biteko.

Inaelezwa kuwa takribani asilimia 34.4 ya idadi ya Watanzania wote ni vijana ambao ni sawa na asilimia 56 ya nguvu kazi ya Taifa na asilimia 46 ya idadi ya watu wote duniani ni vijana walio chini ya umri wa miaka 25. 
‘’Wote mtakuwa mashahidi kinachoendelea duniani kote, amani imepungua, vifo vimeongezeka, matukio ya uovu yamekithiri na baadhi ya mataifa hayana amani kwa sababu yana migogoro na mivutano ya kisiasa. Ni vyema mkatambua kwamba ninyi vijana wa Tanzania pamoja na wenzenu duniani kote mna jukumu kubwa la kutoa hamasa ya kushiriki katika kujenga na kuilinda amani, na msimruhusu mtu yoyote kuichezea tunu hiyo muhimu kwenye mustakabali wa Taifa lolote Duniani.’’Amemalizia Dkt. Biteko.