Mwenyekiti wa Mkutano huo, Ummy Mwalimu (Katikati)
Mkutano huo ulifanyika juzi jijini Nairobi, Kenya ambapo pia ulijadili masuala mbalimbali yahusuyo sekta ya afya kwa ujumla.
Katika taarifa yake aliyoituma kwa vyombo vya habari, Waziri Ummy alisema mkutano huo ulihudhuriwa na Mawaziri wa Afya wa Kenya, Burundi, Uganda pamoja na Mwakilishi wa Waziri wa Afya wa Rwanda.
“Mkutano huo ulitanguliwa na kikao cha wataalam na kikao cha makatibu wakuu wa wizara za afya katika nchi wanachama vilifanyika kuanzia Novemba 14 hadi 17, mwaka huu,” alisema.
Alisema mambo makubwa yaliyojadiliwa na kupitishwa katika mkutano huo ni Sera ya Afya ya EAC (EAC Regional Health Policy) na Sera, Mwongozo na Mkakati wa EAC wa Afya ya Mama, Mtoto na Vijana (Intergrated EAC Reproductive, Maternal, Newborn, Child and Adolescent Health Policy Guidelines and Strategic Plan).
Waziri Ummy alisema mkutano huo wa Mawaziri pia ulichambua na kupitia taarifa ya Makatibu Wakuu wa Wizara za Afya ambapo ulieleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa maagizo ya mawaziri wa afya ikiwemo kuanzishwa kwa mpango wa pamoja wa kusimamia dawa, mpango wa pamoja wa kukagua Vyuo Vikuu vya Afya pamoja na mpango wa pamoja wa huduma za UKIMWI/VVU.
“Taarifa ya Ukaguzi wa Vyuo Vikuu vya Afya vya Tanzania itawasilishwa katika Kikao cha 14 cha Mawaziri wa Afya wa EAC kitakachofanyika Bujumbura Machi, mwakani,” alisema.