Ijumaa , 30th Sep , 2016

Mwelekeo wa ukuaji uchumi barani Afrika unatarajia kukwama zaidi na kuwa asilimia 1.6 mwaka huu ikilinganishwa na asilimia 3 mwaka jana, hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya Benki ya Dunia itolewayo mara mbili kwa mwaka, Africa's Pulse.

Makao Makuu ya Benki ya Dunia

Ripoti hiyo inasema mwelekeo wa ukuaji unatofautiana ambapo baadhi ya nchi ukuaji unakwama huku nyingine uchumi ukikua.

Ripoti hiyo imezitaja nchi za Rwanda, Tanzania na Ethiopia kuwa ukuaji wa uchumi kwa wastani ni zaidi ya asilimia 6 kwa mwaka huku, huku Cote d'Ivoire na Senegal zikichomoza zaidi.

Mchumi mkuu wa Benki ya Dunia kuhusu Afrika, Albert Zeufack amesema chanzo cha kukwama uchumi ni kudorora kwa bei za bidhaa ikiwemo mafuta, hali ngumu ya kifedha na sera za uchumi zisizo makini.

Benki ya Dunia inasema mwelekeo ni kupanua wigo wa bidhaa zinazouzwa pamoja na kuboresha sekta ya kilimo hasa kwa wakulima wadogo ili kuinua vipato vyao na kupunguza umaskini.