Alhamisi , 4th Jun , 2015

Naibu katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii nchini Tanzania Bw. Selestini Gisimba amesema sekta ya utalii hapa nchini na katika nchi za Afrika inakabiliwa na ukosefu wa wataalam licha ya kutangazwa kwa vivutio vya utalii vilivyopo katika nchi.

Naibu katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii

Akizungumza jijini Dar es salaam mara baada ya kufungua mkutano wa masuala ya utalii kutoka nchi mbalimbali za Afrika na nje ya Afrika kwa lengo la kubadilisha uzoefu Bw. Gisimba ametolea mfano wa Tanzania na kusema kwamba mara nyingi watalii wanapokuja na kufanyiwa tathmini wamekuwa wakieleza kwamba Tanzania imekuwa haifahamiki licha ya kuwa na vivutio vizuri vya utalii.

Kwa upande wake kaimu makamu mkuu wa chuo kikuu cha Dar es salaam Profesa Florence Luoga ambao ndiyo waratibu wa mkutano huo amesema kuna haja sasa kwa vyuo vya elimu ya juu hapa nchini kuwa na mafunzo yanayohusiana na sekta ya utalii kwa kuwa chuo cha utalii pekee hakitoshelezi mahitaji ya nchi nzima.

Amesema iwapo vyuo vikuu hapa nchini vitakuwa mstari wa mbele kutoa elimu ya masuala ya utalii Tanzania inaweza kuwa na watalaam ambao watawezesha utalii kukua na kuongeza pato la taifa.