Ijumaa , 25th Sep , 2015

Serikali ijayo imetakiwa kuweka msingi ulio imara kikatiba ili kulinda ubunifu wa vijana ambao kwa kiasi kikubwa umekuwa ajira tegemezi, ilikuweza kutatua tatizo la ajira kwa vija alinaloikabili nchi yetu.

Wito huo umetolewa na Meneja wa mradi wa shirika la maendeleo kwa vijana (Restless Development) Oscar Kimaro, alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha super mix kinachorushwa na East Africa Radio, kuzungumzia ni jinsi gani serikali ijayo itasimamia maslahi ya vijana kikatiba.

Bwn. Kimaro amesema katiba iliyopita ilikuwa na mapungufu kwani ilikuwa na ukosekanaji wa uwakilishi wa matakwa ya makundi mbali mbali hususan vijana, hivyo kuna haja kubwa kwa katiba na serikali ijayo, iweke katiba ambayo itasimamia matakwa ya vijana katika nyanja zote.

Pia Bwn. Kimaro ameitaka serikali kutoa elimu bora kwa vijana itakayoendana na soko la ajira, na kukuza ubunifu wao kwa kuweka haki miliki za kazi zao za kisanaa, ili kuikabili changamoto ya kutokuwa na haki miliki ya kazi zao.

Pamoja na hayo Bwn. Kimaro amewataka vijana kutumia fursa iliyopo kushiriki katika maamuzi, na pia kushirikishwa katika mifumo ya utawala, na kutolaumu mfumo fulani bila kuwajibika na kuwawajibisha pale wanapokwenda kinyume.

Kwa upande wa watu waliotoa maoni kwenye kipindi hicho wameitaka serikali kuweka kipaumbele kwa ajira za wazawa kwenye sekta ya uwekezaji, na kuangalia upya sera za kumiliki ardhi ili waweze kutengeneza ajira zao binafsi na kuwekeza.