EATV imetembelea vituo kadhaa kikiwemo cha mtaa wa Mkunduge kilichoko Tandale ambako kulizuka vurugu zilizo sababisha mtendaji wa kituo hicho kusitisha zoezi hilo tofauti na katika vituo vya shule za msingi za Shekilango na Buguruni ambazo zoezi hilo linaendelea kwa utulivu ingawa baadhi ya makarani wamelalamika kuhusu maudhurio hafifu.
Zoezi la uandikishwaji wapiga kura katika mtaa wa Mkunduge kata ya Tandare jijini DSM limelazimika kufungwa kwa muda baada ya mtu asiyejulikana ni mkazi wa mtaa gani kuvamia kituoni hapo na kuchana daftari la kuandikia wapiga kura wa eneo hilo hatua ambayo imelazimu polisi kusitisha zoezi hilo.
Kaimu Afisa Mtendaji mtaa huo bi Joyce Msai amekiri kutokea kwa tukio hilo na amesema kuwa swala hilo wamelifikisha kwenye vyombo vya dola.
EATV imetembelea pia mtaa wa Tandare kwa Tumbo ambako hali haikuwa tofauti sana na mtaa wa Mkunduge kwani aliibuka kijana asiyefahamika akitaka kujiandikisha kwenye daftari hilo kwa nguvu kabla ya kudhibitiwa na wasimamizi wa zoezi hilo.
Kaimu Mtendaji wa kata ya Tandale aliyejitambulisha kwa jina moja la Dalia alipopigiwa simu kwaajili ya kutoa ufafanuzi wa swala hilo alikataa kuzungumza kwa madai kwamba yeye si msemaji wa swala hilo.
Katika kituo cha Zahanati ya Tandale ambacho vurugu zilizuka katika siku ya kwanza ya uandikishaji, zoezi hilo limeendelea kwa utulivu ingawa lilichelewa kuanza baada ya waandikishaji kuhamishiwa nje kutoka chumba walichokuwa wanatumia.
Baadhi ya wananchi wameonesha kutokujua kinachoendelea, hata baada ya kujiandikisha na wengine wamelalamikia hatua ya zoezi hilo kufanyika katika maeneo ya kutolea huduma za afya na shule hali inayosababisha wananchi kukosa huduma ambazo zingepaswa kutolewa katika maeneo hayo.