Alhamisi , 2nd Jun , 2016

Serikali imesema kuwa itahakikisha kuwa inawakamata wote waliohusika na mauaji ya kinyama ya watu wanane Mkoani Tanga kwa kuwa ina mkono mrefu huku ikiwaomba wafiwa kuwa na subira katika kipindi ambacho serikali inafanya uchunguzi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akitoa maelekezo kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Leonard Paulo (kulia),

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Hamad Yusuph Masauni baada ya kutembelea wananchi wa Kitongoji cha Kibatini Kata ya Mzizima Jijini Tanga ambapo aliongoza na wakuu wa vikosi vya usalama nchini.

Vingozi waliotembelea eneo hilo jana ni Pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenerali Davis Mwamunyange, Mkuu wa jeshi la Polisi Inspekta Jenerali Ernest Mangu, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela na viongozi wengi waandamizi wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Kwa upande wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenerali Davis Mwamnyange amesema msiba huo ni wa Watanzania wote na kusisitiza kwamba kila alieshiriki mauaji hayo kwa namna moja ama nyingine atakamatwa.

Katika hatua nyingine baadhi ya wakazi wa kitongoji cha kibatini wameanza kuyakimbia makazi yao kutokana na hofu ya kuongezeka kwa matukio ya uvamizi,uporaji mali unaombata na mauaji katika eneo hilo.