Jumanne , 2nd Dec , 2014

Taasisi ya Sekta Binafsi nchini -TPSF imeanzisha Mfuko Maalum wa kuwawezesha wanawake kugombea ubunge wa kuchaguliwa.

Uanzishwaji wa mfuko huo jijini Dar es salaam ni matokeo ya Mkutano wa pamoja wa mashauriano baina ya TPSF na Wabunge Wanawake Wenye majimbo nchini, uliokusudia kutafuta namna ya kuwawezesha wabunge wanawake kushiriki na kushinda majimbo katika uchaguzi mkuu ujao.

Akizungumza katika mkutano huo Mbunge wa Hanang', ambaye pia ni Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji Dr. Mary Nagu amesema wanawake hawana budi kuwania nafasi za ubunge wa kuchaguliwa, na kusisitiza kuwa ili harakati zao zifanikiwe ni lazima ziungwe mkono na wanaume.

Mapema Mwenyekiti wa TPSF Dr. Reginald Mengi aliwahamasisha wanawake nchini kujiamini kuwa wanaweza kufanya makubwa, iwapo harakati zao za kupigania usawa zitawashirikisha pia wanaume.

Kuhusu Mfuko huo Dr Mengi amesema mtaji wake wa kuanzia utakuwa wa kiasi cha shilingi milioni 100, ambapo jumla ya shilingi milioni 19.5 ziliahidiwa kuchangwa na wanachama wa TPSF waliohudhuria mkutano huo.

Wakati wa mkutano huo Baadhi ya wabunge wanawake na wanachama wa TPSF waliotoa maoni mbalimbali kuhusu namna ya kuendeleza ushirikiano baina yao.