![](http://eatv.tv/sites/default/files/styles/detailpageimg/public/news/2016/03/14/hu.jpg?itok=-uZ00LNp×tamp=1473438562)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Total Afrika Mashariki, Javier Rielo Ikulu jijini Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefanya mazungumzo leo Ikulu jijini Dar es Salaam na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Total Afrika Mashariki, Bw. Javier Rielo, Kampuni ambayo itaanza ujenzi wa Mradi wa Bomba la kusafirisha Mafuta kutoka nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania.
Bw. Javier Rielo amemwambia Rais Magufuli kuwa mradi huo utahusisha ujenzi wa bomba lenye urefu wa kilometa 1,410 ambalo litasafirisha mafuta ghafi mapipa 200,000 kwa siku kutoka ziwa Albert nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga na utarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja 1,500 na ajira zisizo za moja kwa moja 20,000.
Katika Mazungumzo hayo Bw. Javier amemueleza Rais Dkt. Magufuli kuwa Kampuni yake inatarajia kutumia kiasia cha dola za Marekani karibu bilioni 4 kwa ujenzi huo na ambazo tayari zimeshatengwa.
Pamoja na kuukaribisha uwekezaji huo mkubwa kwa Tanzania, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameitaka kampuni hiyo kuharakisha mchakato wa kuanza kwa mradi, na ameshauri muda wa miaka mitatu uliopangwa kuukamilisha mradi huo upunguzwe, ili manufaa yake yaanze kupatikana mapema.