Jumatano , 12th Feb , 2025

Wananchi wa Kata ya Makanya, Wilaya ya Same, Mkoani Kilimanjaro, wameipongeza Serikali kwa kuwapelekea elimu ya fedha ambayo inatarajia kuwa kichocheo cha maendeleo yao ya kiuchumi.

Wananchi wa Kata ya Makanya, Wilaya ya Same, Mkoani Kilimanjaro, wameipongeza Serikali kwa kuwapelekea elimu ya fedha ambayo inatarajia kuwa kichocheo cha maendeleo yao ya kiuchumi.

Mafunzo hayo yamelenga wananchi, wafanyabiashara, wajasiriamali, wakulima, wafugaji, watumishi wa Umma na Binafsi, Watoa Huduma za Fedha ili kufahamua Sheria, Kanuni na Miongozo ya Huduma Ndogo za Fedha na  kufahamu masuala ya Akiba, Mikopo, Uwekezaji wa Fedha, Bima, Matumizi bora ya Fedha na kujipanga na maisha ya baadae/uzeeni.

Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bi. Dionesia Mjema, alieleza kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwaelimisha wananchi kuhusu matumizi sahihi ya fedha, ikiwemo kupanga bajeti, kuweka akiba, na mikopo salama.

“Matatizo mengi ya kifamilia hutokana na changamoto za kifedha, hivyo elimu hii itasaidia kuboresha maisha ya familia nyingi, na ndoa nyingi zinazovunjika hutokana na mzigo wa madeni. Nahimiza ushirikiano kati ya wanandoa katika kupanga matumizi ya mikopo”. alisema Bi. Dionesia

Diwani wa Kata ya Makanya, Mhe. Damari Kangalu alitoa shukrani kwa Wizara ya Fedha kwa kuwapelekea mafunzo hayo muhimu kwa wananchi wake na kwamba elimu hiyo itawasaidia wananchi kuepuka mikopo umiza na kuimarisha hali yao ya kifedha. 

“Hata wale wenye kipato kidogo wanaweza kuweka akiba na hatimaye kuwekeza ili kupata faida kubwa zaidi kwa muda mrefu. Hili litasaidia kuinua uchumi wa familia na jamii kwa ujumla”. alisema Bw. Kangalu

Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, alieleza kuwa Wapo Watoa huduma za fedha wasio waaminifu na hawatoa taarifa sahihi za huduma zao kwa wateja hali hiyo imesababisha watumiaji wengi kutojua wajibu wao na kusababisha migogoro kati yao, hivyo kila Mtoa huduma ahakikishe kabla ya kutoa huduma wanatoa elimu ya fedha nakuweka wazi wajibu wa Mtoa Huduma na Mteja kwenye mkopo au huduma anayotoa.

Wananchi wa Kata ya Makanya walieleza kufurahishwa na mafunzo hayo yanayotolewa na Wizara ya Fedha pamoja na Taasisi zake kwa kuratibu elimu hiyo muhimu. 

Mafunzo hayo yanatolewa katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Kilimanjaro, zikiwemo Wilaya ya Same, Mwanga, na Rombo.

Kupitia juhudi hizo, wananchi wengi zaidi wataweza kutumia fedha zao kwa ufanisi, kujikwamua kiuchumi, na kujenga maisha bora kwa siku za usoni.

Timu ya Maafisa kutoka Wizara ya Fedha ilitoa elimu kwa washiriki zaidi ya 700 juu ya usimamizi wa fedha, mbinu za uwekezaji, na umuhimu wa kuweka akiba.