Wakati leo Januari 12 ikiwa ni maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewatakia Watanzania wote kheri ya maadhimisho hayo.
Katika chapisho lake la leo kwenye mitandao ya kijamii, Rais Samia ameandika, “Ninawatakia nyote kheri katika maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Kwa miaka 62 tumeendeleza dhamira ya msingi ya Mapinduzi ya kujenga jamii ya watu huru, yenye utu, yenye maendeleo, umoja, haki, amani na mshikamano,” amesema.
“Sote tunao wajibu wa kuendelea kuzilinda tunu hizi na kuzirithisha kwa vizazi vijavyo, kama tulivyorithi toka kwa waasisi wetu,” ameongeza.
Mapinduzi ya Zanzibar yalitokea asubuhi ya Januari 12, 1964 ambapo kundi la wanamapinduzi waliokuwa wakiongozwa na John Okello walifanikiwa kuuondoa utawala wa Sultani Jamshid bin Abdullah, ambaye alikuwa akitawala kwa mfumo wa kifalme baada ya Zanzibar kupata uhuru kutoka Uingereza mwezi Desemba 1963.
Baada ya mapinduzi hayo, Kiongozi wa ASP Abeid Karume, akawa rais wa kwanza wa Visiwa hivyo ambavyo viliungana na iliyokuwa Tanganyika kwa wakati huo na kuunda taifa la Tanzania mnamo April 26, 1964.



