Studio ya redio
Vituo hivyo vinakabiliwa na mapungufu ikiwemo wafanyakazi kufanyishwa kazi bila mikataba ya ajira,vituo kukosa ubunifu wa kutafuta habari na matukio na kuwa na watangazaji wa darasa la saba.
Akizungumza wakati wa Mkutano wa Watoa huduma za maudhui zikiwemo Redio, Tv na Mitandao ya Kijamii uliofanyika Machi 8, 2019 Jijini Mwanza, Mkuu wa TCRA Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo amevitaka vituo vya redio kufanya marekebisho vinginevyo vituo hivyo vitaamuriwa kusitisha huduma.
Amesema hivi karibuni Kamati ya Maudhui ya TCRA ilifanya ukaguzi kwenye vituo vya Redio takribani 36 vilivyopo Kanda ya Ziwa na kubaini kuwa vingi vina hali mbaya ya kiundeshaji na kiutendaji.
"Mapungufu mengine ni vituo kukosa vyoo na kama vipo basi ni vichafu lakini cha kushangaza kwenye ratiba yao ya vipindi wana vipindi vya afya, pia baadhi ya studio hazina Sound Proof, viyoyozi hali inayopelekea watangazaji kufungua madirisha pale wanapozidiwa na joto", amesema Mhandisi Francis Mihayo.
"Baadhi ya vituo vimekosa ubunifu wa kutafuta habari na matukio kunakopelekea ku kubadilisha ratiba ya vipindi bila kutoa taarifa TCRA, mfano vipo vituo vya redio Wamiliki wake huamua kwa matakwa yao wenyewe kubadilisha vipindi kwa kuwaamrisha wakuu wa vipindi bila kufuata taratibu", ameongeza.
Akiendelea kutaja mapungufu hayo, amesema baadhi ya vituo vya redio havina mlinzi hata mmoja, kutokuwa na mazingira rafiki ya kufanyia kazi, vituo kutolipia leseni kwa mujibu wa sheria na kushindwa kutoa taarifa za kweli pale TCRA inapoomba taarifa kutoka kwa watoa huduma.
Kutokana na mapungufu hayo, Mhandisi Mihayo amesema baada ya miezi minne iliyotolewa kujirekebisha wataamuru vituo vifungwe endapo havitatekeleza.