Jumatano , 6th Sep , 2023

Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba, ameiambia Benki ya Dunia kwamba serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara ili kuiwezesha sekta binafsi kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa nchi na kuwezesha upatikanaji wa fedha za kigeni.

Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba

Dkt. Nchemba, amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Benki ya Dunia, ukiongozwa na Mkurugenzi anayesimamia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika Hassan Zaman Jijini Dar es Salaam.

Ameiomba Benki hiyo kuharakisha upatikanaji wa zaidi ya dola za Marekani Milioni 500 ifikapo mwezi Novemba mwaka huu ili fedha hizo zisaidie nchi kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa dola za Marekani katika mzunguko wa fedha nchini hali inayochangia mfumuko wa bei na kukwamisha uagizaji wa bidhaa muhimu kutoka nje ya nchi ikiwemo mafuta.

Katika mkutano huo wamejadili masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Benki hiyo, ikiwemo namna ya kuisadia nchi kukabiliana na athari za upungufu wa dola za Marekani katika mzunguko wa fedha, ili kulinda ukuaji wa uchumi.

Amesema kuwa serikali kupitia Bunge, limepitisha mabadiliko mbalimbali ya sheria na kanuni zitakazowezesha kuvutia uwekeaji wa mitaji na teknolojia ambapo sheria kadhaa zimefanyiwa marekebisho na sheria nyingine ya masuala ya ununuzi wa umma itajadiliwa bungeni ambapo maboresho ya sheria hiyo yatachochea zaidi uwekezaji.

Aidha, Dkt. Nchemba ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuidhinisha upatikanaji wa fedha kwenye miradi 8 yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 2.16 kati ya miradi 26 yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 5 ambayo Serikali imewasilisha kwenye Benki hiyo, na kwamba miradi hiyo itakapokamilika itakuwa na matokeo chanya katika kukuza uchumi na maendeleo ya watu.