Jumatatu , 8th Aug , 2022

Serikali ya Tanzania imesaini makubaliano ya shilingi bilioni 23.7 ya ushirikiano na serikali ya shirikisho la Ujerumani kwa ajili ya kudhibiti uharibifu wa wanyamapori na vifo vinavyosababishwa na wanyamapori kama Tembo katika jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi.

Kushoto ni Balozi wa Ujerumani nchini Regina Hess na kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Emmanuel Tutuba

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Emmanuel Tutuba,  amesaini mkataba wa ushirikiano na serikali ya Ujerumani ambapo bilioni 14.2 ni kwa ajili ya mradi wa kukabiliana na mwingiliano wa wanyamapori na binadamu, na bilioni 7.1  ni za kusaidia upatikanaji wa haki kwa wanawake na watoto, huku bilioni 2.4 zikielekezwa katika utafiti na maandiko.

"Baada ya kuhifadhi wanayama wetu tunaona wameongezeka na kuvamia wananchi na mashamba ya jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi zetu, sasa sekta ya utalii katika mradi huu imeepewa zaidi ya bilioni 6 ambazo zitaenda kusaidia kukabiliana na athari za mwingiliano wa wanyamapori na binadamu," amesema  Dkt Tutuba 

Akizungumza kwa niaba ya serikali ya shirikisho la Ujerumani, Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania amesema kwamba baada ya  kushirikiana katika miradi ya maji na afya, sasa wanakwenda kusaidia jamii zinazozunguka hifadhi huku viongozi wa Wizara ya maliasili na Utalii pamoja na Katiba na Sheria wakiahidi kusimamia matumizi sahihi ya fedha hizo.