Jumatatu , 11th Dec , 2023

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,  Mhe. Dkt. Doto Biteko  amesema Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye utekelezaji wa  makubaliano ya Ajenda 2063, ya kuifanya Afrika kuwa mahali pa ndoto yetu kuelekea Afrika tuitakayo.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akizungumza na Rais wa Jamhuri ya Botswana, Mhe. Dkt. Mokgweetsi Masisi wakati alipofika ofisini kwake kwa ajili ya kuwasilisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipomwakilisha kwenye Mkutano wa Ajenda 2063 uliohusisha Wakuu wa Nchi za Afrika

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,  Mhe. Dkt. Doto Biteko kwenye Mkutano wa kujadili utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa na Wakuu wa Nchi juu ya Ajenda 2063 kwa nchi za Afrika, alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye mkutano huo jijini Gaborone, Botswana, ulioenda sambamba na maadhimisho ya Tamasha la KUSI.

Dkt Biteko alisema kuwa,  kimsingi Tanzania imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa Ajenda hiyo ikiwemo  masuala ya amani, usalama na demokrasia kupewa kipaumbele kwenye  nchi, kuunganisha miradi mbalimbali ya maendeleo na nchi za Afrika ikiwemo ule wa SGR, pamoja na miradi ya umeme kupitia nchi za Kenya, Uganda, Ethiopia, na Zambia, na kufungua fursa za kiuchumi kwa nchi za Afrika.

"Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika itaendelea kutekeleza, kusimamia,na kuendeleza harakati hizi za kuifanya Ajenda hii kutimiza Dira ya Afrika tuitakayo. " Alisisitiza Mhe. Dkt. Biteko

Ajenda ya Afrika 2063 Afrika tuitakayo imebeba vipaumbele Saba  ambavyo ni pamoja na kuleta Afrika pamoja kwenye masuala ya Maendeleo, kuunganisha Bara la Afrika kwenye masuala ya kisiasa kwa kutumia tunu za Afrika, Utawala  Bora na unaozingatia sheria, Demokrasia, na Haki, Kuilinda Afrika, Afrika yenye mwelekeo wa utamaduni wake na Maadili, Afrika itakayowaletea Maendeleo watu wake, kwa manufaa ya wanachi wa Afrika.

Aidha Mhe Dkt. Biteko alishiriki mjadala wa Marais kutoka Afrika kuhusu Ajenda ya umoja wa Afrika 2063 ijulikanayo kama Africas  Agenda 2063 inayotoa mwelekeo wa Afrika kutimiza ndoto zake na kuifanya Afrika waitakayo, mjadala uliohusisha Rais wa Jamhuri ya Watu wa Botswana, Mhe. Dkt. Mokgweetsi Masisi, Rais wa Zimbabwe Mhe. Emmerson Mnangagwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. Dkt. Edouard Ngirente akimwakilisha Mhe. Rais, Paul Kagame, na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Doto Biteko, akimwakilisha Mhe. Dkt Samia suluhu Hassan.