Alhamisi , 3rd Nov , 2016

Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuboresha huduma za uzazi wa mpango nchini tofauti na kipindi cha nyuma ili kuondoa idadi ya ongezeko kubwa la watu na kupunguza vifo kwa wajawazito na watoto kwa mujibu wa sera ya afya ya mwaka 2007

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akifungua mkutano wa bodi kwa nchi zilizoamua kuongeza idadi ya watu wanaofahamu uzazi wa mpango kundi linalojulikana kama "FP 2020 Reference Group.

Amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuboresha huduma za uzazi wa mpango nchini tofauti na kipindi cha nyuma ili kuweza kuondoa idadi ya ongezeko kubwa la watu na kupunguza vifo kwa wajawazito.

Aidha Waziri Ummy amesema kuwa mkutano huo unafanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika na hususani katika ardhi ya Tanzania hii ni kutokana na mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika eneo hili la uzazi wa mpango .

Waziri Ummy alieleza kuwa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Magharibi mwa nchi kumekuwa na ongezeko la uelewa na utumiaji wa huduma za uzazi wa mpango kama vile mkoa wa Mara ambako kuna ongezeko la utumiaji kutoka asilimia 10 hadi asilimia 29 kuanzia mwaka 2010 hadi 2015 na katika mkoa wa Kagera kumekuwa na ongezeko kutoka asilimia 24 hadi asilimia 39.

Mkutano huo wa siku tano ulioanza Oktoba 31 hadi Novemba 4 mwaka huu unahudhuriwa na wajumbe na wadau kutoka nchi mbalimbali duniani ikiwa na lengo la kujadili fursa mbalimbali na changamoto zilizopo katika eneo la afya ya uzazi wa mpango duniani.