Jumatano , 9th Aug , 2023

Tanzania na Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi wa Umoja wa Falme za Kiarabu zimetiliana saini mkataba wa mkopo nafuu wa dola za Marekani milioni 30 sawa na shilingi bilioni 70 za Tanzania kwa ajili ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa KV 220 kutoka Benaco hadi Kyaka na upanuzi wa

Waziri wa Fedha Dkt Mwigulu Nchemba akitiliana saini mkataba wa mkopo huo na Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi wa Umoja wa Falme za Kiarabu

kituo cha kupoza umeme cha Kyaka mkoani Kagera.

Mkataba huo umetiwa saini makao makuu ya mfuko huo Mjini Abu Dhabi na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, kwa niaba ya Serikali, na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi (Abu Dhabi Fund for Development), Mhe. Mohammed Saif Al Suwaidi.

Waziri Nchemba amesema kuwa mradi huo utahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme umbali wa kilometa 167 kutoka Benaco hadi Kyaka na kwa mujibu wa Wizara ya Nishati mradi huo utakapokamilika unatarajia kugharimu dola za Marekani milioni 119.4.

"Mkopo huu tuliosaini utachangia nguvu zilizotolewa na mifuko mingine ukiwemo OPEC Fund for International Development uliotoa dola za Marekani milioni 60, Mfuko wa Maendeleo wa Saudia uliotoa dola za Marekani milioni 13 na serikali ya Tanzania iliyochangia dola za Marekani milioni 2.4," amesema Dkt. Nchemba

Imeelezwa kuwa, kukamilika kwa mradi wa umeme wa Benaco-Kyaka, kutaimarisha hali ya upatikanaji umeme katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ambapo kumekuwa na changamoto ya kuwepo kwa umeme pungufu na usio wa uhakika na pia kuufanya mkoa wa Kagera kuanza kutumia umeme wa gridi ya Taifa badala ya kutumia umeme kutoka nchi jirani ya Uganda.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi, Mohammed Saif Al Suwaidi, amesema kuwa mfuko wake utaendelea kufadhili miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Tanzania ili nchi ifikie malengo yake ya kuwaletea wananchi maendeleo kuoitia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.

Miongoni mwa miradi ambayo mfuko huo umetoa fedha kwa Tanzania ni pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Wete-Pemba, barabara ya Kidawe hadi Uvinza (km 77), ujenzi wa kiwanda cha Sukari Kagera na mradi wa maji Zanzibar vijijini ambayo imekamilika na hivi sasa wanafadhili ujenzi wa barabara ya Uvinza-Ilunde hadi Malagarasi wenye thamani ya dola za Marekani milioni 15.