Jumanne , 20th Aug , 2024

Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameihakikishia Jumuiya ya Kimataifa na Watanzania kwa ujumla kwamba serikali inaendelea kuweka na kuboresha mazingira ya uwekezaji ikiwemo kuboresha mifumo yake ya kodi. 

Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba

Dkt. Nchemba ameyasema hayo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam, wakati akiagana na Balozi wa Uswisi aliyemaliza muda wake wa ubalozi hapa nchini Didier Chassot.

Amesema kuwa Rais Samia, ameunda timu ya wataalam ya kupitia na kuja na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha mifumo yake ya kodi ili kuvutia zaidi biashara na uwekezaji nchini.

Dkt. Nchemba amefafanua kuwa pamoja na kuundwa kwa timu hiyo, serikali pia imechukua hatua kadhaa za kuboresha ya kielektroniki ya ukusanyaji kodi inayosaidia kukusanya mapato yake kwa ufanisi na kuondoa usumbufu kwa walipa kodi.

Amesema kuwa lengo la kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja na kuimarisha mifumo ya kodi ni kuhakikisha kuwa idadi ya walipakodi inaongezeka hatua itakayosaidia pia kuiwezesha Serikali kupunguza viwango vya kodi ya ongezeko la thamani siku za usoni kwa sababi walipakodi watakuwa wengi.

Kwa upande wake Balozi wa Uswisi aliyemaliza muda wake hapa nchini, Didier Chassot, ameipongeza serikali kwa uamuzi huo wa kupitia mifumo ya kodi na kwamba anaamini Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini watapata pia nafasi ya kuzungumza na kujadiliana na Serikali kuhusu masuala hayo kama walivyoomba