Alhamisi , 22nd Mei , 2014

Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Nchi Kavu na Majini, SUMATRA Kanda ya Mashariki nchini Tanzania imezitaka kampuni zinazotoa huduma ya usafiri kuelekea mikoani na nchi za jirani kutokea Dar-es-Salaam kutii agizo la mabasi yote kupulizwa dawa kuua mbu.

Baadhi ya mabasi yanayofanya safari zake kutoka kituo kikuu cha mabasi Ubungo na ambayo Sumatra imekuwa ikisisitiza kuwa yapulizwe dawa kuua mbu wanaosambaza homa hatari ya Dengue.

Akizungumza leo jijini Dar-es-Salaam Afisa Mfawidhi wa SUMATRA kanda ya mashariki Bw. Conrad Shio amesema zoezi hilo ambalo lilikuwa limalizike jana litamalizika kesho asubuhi na kusisitiza wamiliki wa mabasi hayo kuhakikisha kabla hayajaanza safari za kwenda mikoani na nje ya nchi yawe yamepuliziwa dawa hiyo.

Bw. Shio amesema mpaka sasa zaidi ya mabasi 500 yameshapuliziwa dawa hiyo ambapo kesho ni zoezi la kumalizia yaliyobaki ni vema wamiliki wa mabasi hayo wakahakikisha yanakuwepo katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi mapema asubuhi tayari kwa zoezi hilo.