Ijumaa , 25th Nov , 2022

Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kimetoa tuzo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo kwa kutambua na kuthamini mchango wake mkubwa wakati akiwa mwanafunzi chuoni hapo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo, akipokea tuzo

Dkt. Jafo ni miongoni mwa wanazuoni wachache waliopata tuzo hiyo akifanya vizuri katika masomo yake na kuleta tija na mchango mkubwa kwa jamii tangu ahitimu masomo yake chuoni hapo mwaka 2001.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka chuoni hapo, ameipata tuzo hiyo kutokana na mchango wake mkubwa kwa jamii alioufanikisha wakati alipokuwa anatimiza majukumu yake katika jamii kwa vipindi tofauti kutokana na chuo hicho kufuatilia mwendendo na tabia za wanazuoni wao waliohitimu chuoni hapo ili kubaini mchango wao katika jamii. 

"Hii ni heshima kubwa sana kwangu, familia yangu na Taifa langu, niliwahi kusoma hapa miaka iliyopita katika ngazi ya shahada na wanafunzi wapo wengi sana lakini waliona wanipatie mimi hasa kwa mchango mkubwa nilioutoa katika nyanja mbalimbali wa jamii," amesema Dkt. Jafo.

Aidha, Dkt. Jafo ametajwa kuwa ameleta mchango mkubwa alipokuwa katika nafasi ya mtaalamu wa kilimo wa Halmashauri ya Kisarawe mkoani Pwani kwa mwaka 2001 hadi 2005.

Pia taarifa ya chuo hicho imeonesha kwamba alikuwa Mtanzania wa kuigwa kwa kuchapa kazi kwa kuleta matokea alipokuwa akifanya kazi katika Shirika la Kimataifa la Plan International Ofisi ya Tanzania kwa nafasi ya Meneja wa Miradi.

Katika nafasi ya ubunge amehudumia vyema wananchi wake sambamba na kuliwakilisha Bunge la Tanzania katika Bunge la Jumuia ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ikiwa ni pamoja na kuwa Mweka Hazina wake.

Eneo lingine kubwa lililompa heshima hiyo ni kuwa kiongozi mwenye ari, mnyenyekevu, na anaye jituma kwa moyo mkubwa bila ya kuchoka kwa ajili ya jamii alipokuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI) na katika nafasi yake ya sasa ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).