Jumatatu , 22nd Aug , 2016

Idadi ya mauzo katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) imepanda kwa 57% kutoka mauzo yenye thamani ya shilingi bilioni 2.1 hadi bilioni 3.3, kwa mujibu wa taarifa ya mwenendo wa biashara katika soko hilo zilizokusanywa kwa wiki moja iliyopita.

Afisa Mauzo wa DSE Bi. Mary Kinabo

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam leo, Afisa Mauzo wa Soko hilo Bi. Mary Kinabo amesema katika kipindi hicho, idadi ya hisa zilizouzwa na kununuliwa nayo imeongezeka kwa asilimia 34 kutoka hisa milioni 1.6 hadi hisa milioni 2.2 huku ukubwa wa mtaji wa soko ukiwa umepanda kwa asilimia 0.67 kutoka mtaji wenye thamani ya shilingi trillioni 23.2 hadi shilingi trilioni 23.4.

Ukubwa wa mtaji wa makampuni ya ndani umebaki kwenye kiwango kile kile cha shilingi trilioni 8.4 ambapo kiashiria cha sekta ya viwanda kikiwa kimeshuka kwa pointi 19.47 wakati kiashiria cha sekta ya huduma za kibenki na kifedha kikipanda kwa pointi 29.89 huku kiashiria cha sekta ya huduma za kibiashara ikiwa imebaki vilevile ilivyokuwa juma lililopita.