Jumapili , 21st Feb , 2016

Waziri wa nchi ofisi ya Rais TAMISEMI George Simbachawene amesema serikali inaangalia namna ya kuunda upya shirika la elimu kibaha (KEC) ili liweze kuendana na mahitaji ya jamii kwa sasa.

Waziri wa nchi ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe.George Simbachawene

Waziri huyo amesema hayo alipokuwa katika ziara ya kutembelea shirika hilo ambapo pamoja na ziara hiyo alipata fursa ya kuongea na kusikiliza kero za wafanyakazi wa shirika hilo.

Baada ya kusikiliza kero za wafanyakazi ambazo baadhi ilikuwa ni kukosa kupanda madaraja, vyeo, kukosa kulipwa malipo ya muda wa ziada, waziri huyo alisema amebaini kuwa kuna shida ya kiuongozi hivyo kusababisha shirika hilo kuyumba.

Amesema kufuatia malalamiko kadhaa ya wafanyakazi ataunda timu maalumu kutoka wizarani itakayoanza kazi wiki ijayo ili ipite kila idara katika ofisi za shirika hilo na kukusanya kero na maoni kusaidia shirika hilo kuboreshwa ili liweze kwenda na mabadiliko ya sasa.

Waziri Simbachawene alisema shirika hilo ni tajiri na lina fursa nyingi za kimaendeleo hivyo wafanyakazi wake hawakupaswa kulalamika shida huku watu wachache wakijinufaisha.

Aidha waziri huyo alimwagiza mkurugenzi wa shirika hilo Syprian Mpemba kuhakikisha shirika linajiendesha lenyewe badala ya kusubiri pesa kutoka serikalini kwani ziko fursa nyingi ambazo zikitumika vizuri zitasaidia kuendesha shirika hilo.