Jumanne , 2nd Jan , 2018

Klabu ya Simba SC ambao ni vinara wa ligi kuu soka Tanzania Bara leo inatarajia kupata nguvu mpya kwenye eneo lake la ulinzi kwa kuanza kuwatumia mabeki wake Shomari Kapombe na Asante Kwasi.

Simba SC huenda ikaanza kuwatumia nyota hao leo kwenye mchezo wake wa kwanza wa michuano ya Kombe la Mapinduzi Visiwani Zanzibar itakapocheza na timu ya Mwenge.

Kapombe na Kwasi jana wamefanya mazoezi ya mwisho hivyo kocha wa timu hiyto Juma Masoud, anaweza kuamua kuwaanzisha. Kapombe alikuwa majeruhi kwa muda mrefu tangu asajiliwe kutoka Azam FC hajaitumikia Simba kwenye michezo ya ligi.

Simba SC kupitia ukurasa wake wa Instagram imethibitisha kuwa wachezaji hao wapo tayari kwaajili ya michuano hiyo. Asante Kwasi ambaye ni raia wa Ghana amesajiliwa katika dirisha dogo lililomalizika hivi karibuni.

Klabu hiyo ya Msimbazi  itaanza rasmi michuano ya Mapinduzi Cup leo  dhidi ya Mwenge. Mchezo huo utapigwa saa 10:30 jioni kwenye uwanja wa Amaan.