Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Bw. Christopher Ryoba Kangoye.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Afisa Afya wa Wilaya hiyo, Emmnuel Saro amesema kuwa wamelazimika kuzifunga shule hizo kutokana na kukosa vyoo vya wanafunzi kujisaidia pamoja na vyoo vilivyopo kutokidhi mahitaji ya kiafya.
Amezitaja shule zilizofungwa kutokana na kutokuwa na huduma ya vyoo kwa wanafunzi kuwa ni pamoja na Shule za msingi Ving’awe, Ising’u na Mang’angu zote zipo katika Kata ya Ving’awe.
Zingine ni shule ya msingi Mazae, Idilo, Bumila na Makutupa
“Ni kweli nimezifunga shule saba hapa Wilayani kutokana na kutokuwa na vyoo kabisa, na zingine kwa sababu ya kutokuwa na vyoo vya kudumu na vilivyopo kujaa, ambapo ni hatari kwa wanafunzi kutumbukia pia kwa magonjwa ya milipuko kama kipindipindu, kuhara damu, homa za matumbo na magonjwa mengine mengi yanayosababishwa na uchafu,” alisema Saro.
Ameongeza kuwa, “Na ukizingatia huu ni msimu wa masika mvua zinavyonyesha hali siyo nzuri, kuna shule ambazo vyoo vyake vimeanguaka, hapo huoni ni hatari kwa watoto wanaosoma, pia sasa watoto wanajisaidia vichakani na kuchafua mazingira na pia ni hatari kwani wanaweza kuumwa na wadudu wabaya.”
Saro amesema kuwa alishatoa notisi tangu mapema mwaka jana ili shule hizo zirekebishe au wajenge vyoo vya kudumu lakini hakuna waliofuatilia zaidi ya shule chache zilizoanza lakini hata hivyo bado kuna uzembe hivyo kwa mamlaka ya sheria namba 164 ya mwaka 2006 idara ya Afya inaruhusiwa kufunga shule hizo mpaka watakaporekebisha hali hiyo ya kuwa na vyoo.
Amesema zoezi hilo la ukaguzi wa vyoo linaendelea katika wilaya nzima ili kuhakikisha shule zote zinakuwa na vyoo vya kudumu ili kuepukana na magonjwa ya milipuko.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Mwaija Lipinga amekiri kufungiwa kwa shule hizo kutokana na kukosa vyoo vya kudumu kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi wake.
“Ni kweli shule saba zimefungiwa kwa kutokuwa na vyoo ila nimeshatoa maagizo kwa walimu wakuu na wenyeviti wa vijiji wahakikishe kuwa wanalishughulikia suala hilo kwa haraka ili watoto waweze kurudi madarasani,” Alisema Lipinga