Jumatatu , 26th Jan , 2015

Serikali mkoani Katavi imewaagiza wadau wa uhifadhi wa mazingira kote nchini kusaidia juhudi za serikali za kupanga mipango ya matumizi bora ya ardhi katika mkoa huo ili kudhibiti ongezeko la mifugo mkoani Katavi na uvamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dk Ibrahimu Msengi.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dk Ibrahimu Msengi ameyasema hayo mjini Mpanda kwenye ufunguzi wa mkutano wa wadau wa mazingira kutoka mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma na baadhi ya wadau kutoka taasisi za uhifadhi za kimataifa wanaojadili kuhusu mipango ya matumizi bora ya ardhi.

Amesisitiza kuwa dhana hiyo ya matumizi bora ya ardhi imebaki nadharia bila vitendo wala utekelezaji na hivyo kuathiri usimamizi wa maliasili yakiwemo maeneo yaliyohifadhiwa na misitu ya vyanzo vya maji ambayo ni muhimu kijamii na kiuchumi na kwa maendeleo ya taifa.

Nao baadhi ya wadau wa mkutano huo ulioandaliwa na taasisi ya kimataifa ya uhifadhi wa mazingira ICUN akiwemo mratibu wa semina hiyo Nuru Sarasara na Mratibu wa mradi wa taasisi ya Tuungane, Petro Masolwa na wadau kutoka taasisi zinazotekeleza shughuli za uhifadhi wa mazingira katika mikoa ya ukanda wa ziwa Tanganyika wamesema utekelezaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi utazisaidia jamii kuhifadhi rasilimali zilizoko kwenye maeneo yao, kwani ongezeko la kasi la mifugo katika mikoa hiyo lisipodhibitiwa linaashiria kutoweka kwa misitu katika ukanda wa ziwa Tanganyika katika kipindi cha miaka mitano cha ijayo.

Mkutano huo umekuja wakati mikoa hiyo na hasa Katavi ikikabiliwa na uharibifu m kubwa wa mazingira unaotokana na ongezeko la shughuli za binadamu ambazo zimeathiri mtiririko wa maji ya mto katika na hivyo kuathiri uhifadhi wa wanyamapori katika hifadhi ya taifa ya Katavi na hasa wanyama waishio majini wakiwemo mamba, viboko na samaki.