Alhamisi , 10th Apr , 2014

Kituo cha sheria na haki za binadamu nchini Tanzania LHRC, kimeitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina kubaini sababu za kujeruhiwa kwa wanasiasa wakati wa kampeni mbali mbali za chaguzi zinazofanyika nchini.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC, Jaji Damian Lubuva

Afisa anayeshughulikia masuala ya bunge na uchaguzi wa kituo hicho Bw. Hamisi Mkindi, amesema hayo leo wakati akitoa tathmini ya uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Chalinze mkoani Pwani, uchaguzi ambao mgombea wa chama tawala CCM Bw. Ridhiwan Kikwete aliibuka mshindi.

Katika maelezo yake, Mkindi amesema kumeibuka tabia ya wanasiasa kujeruhiwa kila kunapofanyika chaguzi nchini na kuongeza kuwa matendo hayo sio tu yanaashiria uvunjifu wa amani, bali pia yanakiuka haki za msingi za binadamu kwani yanawatisha wapiga kura kujitokeza kushiriki katika shughuli za kidemokrasia.