Jumatatu , 6th Mei , 2024

Baada ya Serikali kupitia wizara ya uchukuzi kuwasilisha makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/2025 wabunge wameelezea hisia zao kuhusiana na baadhi ya maeneo wanayotoka.

Baadhi ya Wabunge Wakichangia Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi

Wakichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo iliyowasilishwa na waziri husika wamesema pamoja na jitihada za serikali za kuleta maendeleo lakini baadhi ya maeneo yamekuwa kero kwa wananchi.

"Tunaipongeza serikali kwa kuleta maendeleo nchini lakini baadhi ya maeneo yamekuwa kero kwa wananchi wake," Bona Kamoli, Mbunge wa Ukonga.

"Inatubidi kuboresha bandari yetu hata zile pesa zinazopelekwa hazina na kupangiwa kazi nyingine zinatakiwa kurejeshwa ili bandari iwe vizuri," Abubakary Assenga, Mbunge wa Kilombero

"Miundombinu ya mbuga ya Serengeti sio rafiki hali hiyo inasababisha watalii kupata shida wanapotembelea hifadhi zetu," Esther Matiko, Mbunge Viti Maalumu

Kamati ya kudumu ya bunge ya miundombinu ikiwasilisha maoni na mapendeekezo yake imeishauri serikali kuongeza ufanisi na ubunifu katika utendaji wake ili kuboresha huduma skatika sekta ya usafirishaji.

"Kuboresha huduma za sekta ya usafirishaji kutasaidia kuleta maendeleo ya kiuchumi nchini,"  Selemani Kakoso, Mwenyekiti Kamati - Miundombinu

Awali waziri wa uchukuzi akiwasilisha taarifa ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ameliomba bunge liweze kuidhinisha kiasi cha zaidi ya shilingi trilioni 2.7.

"Miradi tuliyopanga kuifanya katika mwaka huu wa fedha ni pamoja na kuboresha miundombinu ya Bandari, SGR, Ukaratabi wa Meli katika ziwa Tanganyika," Prof. Makame Mbarawa, Waziri wa Uchukuzi