Jumatano , 13th Jun , 2018

Serikali imewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa nchini kuhakikisha wanawafanyia uchunguzi watoto wachanga wanaopelekwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya umma ili kubaini kama wamefanyiwa vitendo vya ukeketaji.

Agizo hilo limetolewa leo Jijini Arusha na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyoazimishwa kitaifa jijini humo katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Karume.

Dkt. Ndugulile amesema kutokana na watoto kuendelea kujengewa uwezo kuhusu hasara za ukeketaji wamekuwa wanajitahidi kutoa taarifa sehemu husika hivyo wazazi wameamua kuanzisha mbinu mpya za kuwakeketa watoto wachanga jambo ambalo haliwezi kuvumilika.

 Dkt. Ndugulile ameongeza kuwa ukeketaji bado ni changamoto kubwa nchini ambapo takwimu za mwaka 2015 zimeonesha bado kuna Mikoa mitano ambayo iko juu ya wastani wa kitaifa katika suala la ukeketaji hivyo ni lazima agizo hilo litekelezwe kwa haraka ili kukomesha tatizo hilo.

Ameitaja Mikoa inayoongoza kwa ukeketaji nchini kuwa ni Manyara 58%, Dodoma 47%, Arusha 41%, Mara 32% na Singida 31%.

 Vile vile Dkt. Ndugulile ameelezea kukithiri kwa mimba za utotoni ambapo Mkoa wa Katavi unaongoza kwa 45%, Tabora 43%, Mara 37% na Shinyanga 34.