Jumanne , 6th Oct , 2015

Serikali ya Tanzania ipo katika jitihada ya kuyakomboa maeneo ya wazi ya umma yapatayo 21,328 ambayo yamevamiwa na watu na kujimilikisha kinyume cha taratibu za kisheria.

Naibu Waziri wa Wizara ya ardhi, nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Angela Kairuki.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Wizara ya ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi mheshimiwa Angela Kairuki katika maadhimisho ya siku ya makazi duniani ambayo mwaka huu yamekua na kauli mbiu isemayo maeneo ya uma kwa wote.

Aidha mheshimiwa Kairuki ameongeza kuwa ni wakati sasa kwa mamlaka zinazohusika na upangaji na usimamizi wa miji kuwa na mipango maalum ya muda mrefu (Master Plane) kwa ajili ya maendeleo ya miji yao.

Amesema maafisa mipango miji katika halmashauri wana wajibu wakuzishauri ipasavyo halmashuri katika kuhakikisha miji yao inapangwa kwa kuzingatia uwepo wa maeneo ya umma na kuwachukulia hatua kali wote wanaokiuka sheria za ardhi.

Katika maeneo hayo jiji la Dar es Salaam pekee lina maeneo yaliyowazi ya umma 154 kati ya hayo 104 yamevamiwa na hivyo kufanya maeneo ya umma yaliyohuru kwa D ar es Salaam kuwa 50 tu.