Jumatano , 20th Jul , 2022

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Damasi Ndumbaro amesema wizara yake inaanza kutoa elimu ya Katiba nchi nzima kwa kushirikiana na asasi zisizo za kiserikali kwa lengo la kuonesha mazuri na mabaya   yaliyomo ndani ya katiba hiyo

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Damasi Ndumbaro

Amesema Katiba iliandikwa tangu mwaka 1977 na kwa sasa kuna mazingira tofauti yanayokinzana na Katiba hiyo

Waziri Ndumbaro amesema kumekuwepo na falsafa nyingi kuhusu Katiba hivyo katika kipindi cha mwaka huu watalaam watafanya tathmini kwa kuwa katika mjadala wa Katiba mpya unaoendelea kwa sasa wengi wanaoongea ni wanasiasa na kusahau kwamba wananchi nao wana nafasi yao ya kutoa maoni yao baada ya kuelewa mazuri na mabaya yaliyomo kwenye Katiba

Katika hatua nyingine waziri Ndumbaro ameeleza kuwa serikali inakwenda kujenga taasisi jumuishi za Sheria tofauti na ilivyo kwa sasa na kwa kuanzia wanakwenda kujenga kwenye majiji na kwenye manispaa

Amesema sababu za kufanya hivyo ni kuondoa usumbufu kwa wananchi wanapotaka kupata huduma katika taasisi hizo za kisheria kufanya kazi maeneo tofauti na pale mwananchi anapohitaji Huduma kulazimika kutumia gharama kubwa kuzifikia huduma hizo