Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Harrison Mwakyembe amesema hayo kwa niaba ya Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, kwenye mkutano wa kujadili na kutathmini uchaguzi mkuu wa rais, madiwani na wabunge uliofanyika mwaka jana, kwa lengo la kuja na mapendekezo yatakayosaidia kukuza demokrasia na kuboresha chaguzi zijazo.
Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano wa pamoja baina ya taasisi ya Utafiti na Elimu ya Demokrasia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam - REDET na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu - LHRC.
Kwa mujibu wa Waziri Mwakyembe, waangalizi wanasaidia kuja na maoni na mawazo yanayosaidia serikali kuandaa mazingira ya chaguzi huru na haki na kwamba mchango wa wahisani pia katika kuzisaidia taasisi za ndani kifedha nao unaheshimiwa na kuthaminiwa.
Waziri huyo wa Katiba na Sheria amezishi taasisi za ndani kujadili uchaguzi huo huku wakiweka mbele maslahi ya nchi, sambamba na kuonyesha wapi penye mapungufu, nini kifanyike na jinsi gani kifanyike badala ya kubaki wakilaumu peke yake.
Aidha, Dkt Mwakyembe amezitaka taasisi zinazoshiriki uangalizi wa ndani, kutafuta vyanzo mbadala vitakavyowawezesha kujitegemea kifedha, ili kuwa na uwezo wa kushiriki uangalizi wa uchaguzi hasa pale itakapotokea wahisani wameshindwa kutoa fedha kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kidemokrasia nchini.
Kwa upande wake, mwanasiasa mkongwe na Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba, amesema chaguzi zimesaidia kuongeza hamasa katika demokrasia na kutolea mfano hali ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu uliopita ambapo hata zoezi la kura ya maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) lilionekana kama ndio kampeni kamili za uchaguzi huo.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, hamasa iliongezeka zaidi pale walioshindwa kuteuliwa ndani ya CCM 'walipochepuka' na kwenda vyama vya upinzani, hatua aliyodai kuwa iliongeza hamasa na ushindani katika uchaguzi huo.
Akitumia uzoefu wake katika kusimamia chaguzi mbali mbali barani Afrika akiwa kiongozi wa jopo la waangalizi, Jaji Mstaafu Warioba amesema kila chaguzi zinakuwa na mapungufu yanayohitaji kushughulikiwa na kwamba changamoto zinazoonekana katika chaguzi za hapa nchini zimeonekana pia katika chaguzi mbalimbali na kwamba kamwe Tanzania haiwezi kujigamba kwamba imefikia kilele cha mafanikio ya demokrasia katika uchaguzi.