Jumanne , 6th Aug , 2024

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, amesema uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ukiwepo wa kusafiri nje ya nchi kuvutia wawekezaji umeifanya sekta ya tumbaku kwa miaka mitatu kukua na kufikia uzalishaji wa tani 122,000 kwa mwaka.

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe

Akizungumzia kukua kwa sekta ya tumbaku nchini leo mkoani Morogoro, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alisema Rais Samia ameitendea haki sekta hiyo kwa kuweka mazingira mazuri ya utendaji ikiwemo juhudi zake za kutunga sera sambamba na kufanya safari za nje kwa lengo la kuvutia wawekezaji nchini na kuifungulia sekta binafsi kushiriki kwa ushindani kwenye kuongeza ya kilimo cha tumbaku.

Bashe alisema kwa uamuzi wa Rais kusafiri nje ya nchi kwa lengo la kushawishi wawekezaji, nchi sasa inavuna zaidi ya Dola Milioni 400 kutokana na usafirishaji wa tumbaku duniani. Alisema nchi iliweka lengo la kuzalisha tani 170,000 hadi tani 200,000, lakini wamefikisha tani 122,000, huku maamuzi ya Rais ya zao hilo aliyochukua yakiiwezesha bei kupanda kutoka wastani wa Dola 1.4 hadi Dola 2.4. 

“Kiwanda hiki kilikuwa kinachakata tani 80,000, lakini sasa ni tani 200,000, ambapo ukichanganya na kiwanda kingine nchini, nchi yetu itafikisha tani 300,000 kwa mwaka, ambapo kwa uwekezaji wa Dola Milioni 300 unaofanyika kwenye kiwanda hiki, soko la ajira litaongezeka hadi watu 12,000 katika wilaya ya Morogoro Mjini.” Alisema Bashe.

Kwa mujibu wa Bashe, soko la tumbaku ya Tanzania nje ya nchi, litaongeza mapato kutoka Dola Milioni 600 hadi Dola milioni 700.