Mkuu wa Wilaya wa Wang'ing'ombe mkoani Njombe Estarina Kalisi.
Hayo yamebainishwa na mkuu wa wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe wakati wa uzinduzi wa Saccos ya Vijana Ulembwe Saccos limited ya wilayani humo, amesema kuwa uongozi wa saccos uangalie kwa makini mchanganuo kwa lengo la kukopesha mtu anayeweza kurejesha mkopo.
Alisema kuwa kumekuwa na matatizo ya kuto rejeshwa kwa mikopo katika Saccos nyingi hapa nchini kutokana na wakopaji kuto kuwa na mchanganuo sahihi wa pesa anayokopa.
Amesema kuwa asilimia kubwa ya wananchi wamekuwa wakijiingiza katika mikopo kwa kuiga na kujikuta wakibadilisha sehemu za kukopa kwa kulipa madeni katika Saccos za awali.
Kwa upande wake wananchi na viongozi wa Kijiji Cha Ulembwe ambapo ndiyo makao makuu ya SACCOS hiyo wamewataka vijana kujiunga katika vikundi mbalimbali zikiwemo SACCOS ili kuweza kusaidiwa na serikali katika mikopo yake kwa vijana.
Katibu wa SACCOS amesema kuwa kupitia hapo wataweza kuwakopesha vijana hasa zile pesa za serikali zilizo tengwa kwa ajili ya vijana na wanawake kwa kuwa hapo ni sehemu ambayo ni salama na inaaminika kama anavyeleza.
Afisa mtendaji wa kijiji cha Ulembwe, Peter Luhasi amewataka wananchi hao waliojiunga katika SACCOS hiyo na kupata mkopo wa pembejeo za wakati wa uzinduzi wakawe mabalozi wazuri kwa wenzao ili nao wajiunge, huku diwani wa kata hiyo akipongeza juhudi za wananchi waliojiunga na SACCOS hiyo na kunufaika na matunda ya mikopo.
Aidha mkuu wa chuo cha maendeleo ya jamii Yohanes Chongolo amehimiza wananchi kujitokeza kujiunga ili kuunganisha nguvu katika SACCOS kwa kuwa kwa mwananchi wa sasa bila kukopa hawezi kufanya maendeleo lakini wakiunganisha mitaji yao wataendelea kwa kukopeshana.