Jumapili , 10th Aug , 2014

Sababu ya wanafunzi wengi kutopenda masomo ya sayansi nchini Tanzania imetajwa kuwa ni kukosekana kwa uhusiano wa karibu kati ya matumizi ya sayansi na maisha ya kawaida.

Sababu hiyo imetajwa kudumaza na kupunguza hamasa ya kusoma na kujifunza sayansi kwa idadi kubwa ya wanafunzi, kiasi cha kusababisha baadhi yao waone wanayojifunza shuleni kuwa ni mambo mageni kwao.

Mkurugenzi wa taasisi ya Young Scientists Tanzania Dkt Kamugisha Gozibert, amesema hayo leo wakati akizungumzia Shindano la wanasayansi chipukizi litakalofanyika jijini Dar es Salaam katikati ya juma lijalo.

Dkt Kamugisha amesema mbali ya kuhusisha sayansi na maisha, ameshauri walimu pia kutoa uhuru wa kutosha kwa wanafunzi wao kufanya tafiti za kisayansi hata nje ya mitaala wanayosomea ili kutoa fursa ya kupata vumbuzi nyingi zaidi za kisayansi.

Kwa mujibu wa Dkt Kamugisha, kuna haja pia ya jamii kuachana na dhana kwamba sayansi lazima ifanyike maabara tena kwenye vifaa vya gharama kubwa na kwamba sayansi inaweza kufanyika popote na kwa vifaa vya gharama ya chini vinavyopatikana katika maeneo tunayoishi.

Kwa kuachana na dhana hiyo, Dkt Kamugisha amesema walimu wanaweza kuwaongoza wanafunzi kutumia vifaa na nyenzo zinazopatikana kiurahisi katika maeneo wanayoishi wanafunzi hao badala ya kutegemea maabara na vifaa vya kisasa.