Alhamisi , 15th Dec , 2016

Kamanda wa kikosi cha Usalama Barabarani nchini Mohamed Mpinga, amewataka wananchi kuvumilia hali ya foleni  kubwa inayojitokeza katika barabara za miji mikubwa, ambayo amesema inasababishwa na ongezeko kubwa la magari.

Moja kati ya nyakati za foleni katika barabara za jijini Dar es Salaam

 

Akizungumza na East Africa Radio, Kamanda Mpinga amesema kwa sasa hali ya magari nchini imekuwa na ongezeko kubwa sana, na matokeo yake kuongeza foleni barabarani, na siyo uwepo wa trafiki kama wananchi wengi wanavyolalamika.

“Wananchi wavumilie, idadi ya magari katika jiji la Dar es salaam imeongezeka kwa kiwango kikubwa, mtu yeyote ajaribu kuangalia miaka mitano iliyopita kwenye maeneo ya maegesho, jaribu kutembelea maegesho, hali iko vile vile!?? Kwa hiyo magari yameongezeka lakini barabara ni zile zile”, alisema Kamanda Mpinga.

Mohamed Mpinga - Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani

Pia Kamanda Mpinga amesema kwa upande wa askari wa usalama barabarani wamekuwa wakijitahidi kwa kiasi kikubwa kupunguza foleni barabarani kwa kusaidia kuongoza kwenye mataa, hivyo watu wanaposema hawafanyi kazi wanawakatisha tamaa.

“Askari wa barabarani wamekuwa wakijitahidi sana, siyo kama wanapenda kukaa katikati, tukisema tutoe askari wote siku mbili tu alafu muone itakavyokuwa, kuna wengine wanafika mpaka saa 10 wako barabarani, mnaposema hawafanyi kazi mnakatisha tamaa sana”