Ijumaa , 26th Feb , 2016

Jeshi la polisi mkoani Mara linawashikilia watu saba kwa tuhuma za kumbaka kisha kunyongwa hadi kufa mtoto wa kike mwenye umri wa miaka minne na nusu Mariam Deaogratus ambaye alikuwa mwanafunzi wa shule ya awali ya Makoko katika manispaa ya Musoma.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mara kamishna msaidizi wa jeshi la polisi ACP Philip Alex Kalangi

Kamanda wa polisi mkoa wa Mara kamishna msaidizi wa jeshi la polisi ACP Philip Alex Kalangi, amesema watu hao wamekamatwa siku moja baada ya kutokea kwa tukio hilo la kikatili.

Awali kamanda alisema mtoto huyo alikumbwa na mkasa huo muda mfupi baada ya kuondoka nyumbani kwao jioni ya Februari 23 mwaka huu kwenda shule kwa ajili ya masomo ya ziada, lakini hakuonekana tena hadi saa 2 usiku wa siku hiyo Februari 23, mwili wake ulipokutwa umetupwa katika nyumba ambayo ujenzi wake unaendelea.

Akizungumzia tukio hilo mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Musoma, Zelothe Stephen, amesema vyombo vya dola vitafanya kila njia katika kuhakikisha mtu yeyote ambaye amefanya kitendo hicho cha kikatili anakamatwa na kufikishwa mara moja katika vyombo vya sheria.