Alhamisi , 13th Nov , 2014

Hofu ya kupoteza fursa za kiuchumi, soko la ajira pamoja na ardhi kwa ajili ya shughuli za uzalishaji mali zimetajwa kuwa ni miongoni mwa sababu zinazochangia hofu kubwa ya ushiriki wa Watanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA, Profesa Samuel Wangwe.

Hayo yamo ndani ya ripoti ya matokeo ya utafiti, uliofanywa na taasisi inayoshujighulisha na Utafiti Kuhusu Kupunguza Umaskini ya REPOA, chini ya mradi unaotekelezwa katika nchi Thelathini na Tano barani Afrika wa Afrobarometer, mradi unoangalia mitazamo ya jamii za nchi hizo kuhusu masuala ya kijamii, siasa na uchumi.

Akizungumza mara baada ya kutolewa kwa matokeo ya utafiti huo, Mkurugenzi Mkuu wa REPOA Profesa Samuel Wangwe amesema lengo la kufanya utafiti huo ni kutaka kufahamu mtazamo wa watanzania kuhusu mtengamano wa Afrika Mashariki na namna wanavyoweza kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazopatikana ndani ya jumuiya hiyo.

Kwa mujibu wa Profesa Wangwe, bado elimu inahitajika kwani utafiti umebaini kuwa bado idadi kubwa ya Watanzania hawapo tayari kushiriki katika mtangamano wa Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, mmoja wa watafiti aliyefanya utafiti huo Bw. Contantine Manda amesema kwa kiasi kikubwa watu wanaoishi maeneo ya mipakani ndiyo wenye mwamko wa kushiriki katika jumuiya hiyo, kutokana na manufaa ya moja kwa moja ya kiuchumi wanayoyapata kutoka nchi jirani ambazo ni wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki.

Manda amesema kiwango cha hamasa ya kushiriki katika jumuiya hiyo kinazidi kupungua kwa kadri mtu alivyo mbali na maeneo ambayo Tanzania inapakana na nchi nyingine za Afrika Mashariki, huku suala la ardhi, hofu ya kupoteza ajira pamoja na fursa za kiuchumi zikiwa ni baadhi ya zababu zinazowafanya watanzania waonyeshe hofu ya kushiriki katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.