
Wallace Karia
CHADEMA imesema imemwandikia barua Rais wa FIFA na nakala nyingine ikipitia kwa Shirikisho la Soka Afrika CAF pamoja na ushahidi wa video inayomuonesha akizungumza kauli hiyo.
"Tunaandika barua hii kuelezea masikitiko yetu na kupinga kauli iliyotolewa na Rais wa TFF, Wallace Karia ambayo inaunga mkono uvunjaji wa haki za binadamu, uhuru wa kuzungumza na kuchochea ubaguzi wa kisiasa jambo ambalo ni kinyume na miiko ya mchezo wa mpira wa miguu unaosimamiwa na FIFA," imeeleza sehemu ya barua hiyo ambayo imesainiwa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa chama hicho, Tumaini Makene.
Katika Mkuu Mkuu wa TFF uliofanyika Februari 2 Jijini Arusha, Karia likemea watu wenye tabia alizoziita za ‘u Tundu Lissu’ katika soka, kuwa kamwe hawezi kukubali kuona wakiendelea kukosoa uongozi wa TFF.
Ambapo baada ya mkutano huo, alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu kauli hiyo, Karia alisema, "nimesema kama kuna ‘ma Tundu Lissu’ kwenye mpira, nadhani mnaelewa Lissu anahangaika kwenye vyombo vya habari kuikashifu Serikali na (Michael) Wambura anazungumza kwenye vyombo vya habari kuikashifu TFF na uongozi wa TFF".
Lakini katika kumalizia ufafanuzi wake, Wallace Karia pia aliwaomba msamaha kama kuna watu ambao aliwakwaza kutokana na kauli hiyo.