Jumanne , 7th Oct , 2014

Serikali Mkoani Dodoma imesema imeimarisha ulinzi na usalama kwa ajili ya siku ambapo Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania atakabidhiwa Katiba Inayopendekezwa, iliyopitishwa na Bunge Maalaum la Katiba ikiwa ndio Katiba inayopendekezwa.

Rais wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Rehema Nchimbi amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika tukio hilo la kihistoria linalotarajiwa kufanyika hapo kesho katika uwanja vya Jamhuri.

Tukio hilo linatarajiwa pia kuhudhuriwa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Ally Mohamed Shein pamoja na viongozi mbalimbali wa kitaifa ikiwa ni pamoja na Viongozi wa Dini, Mabalozi, Makundi ya Kijamii pamoja na Wananchi.

Aidha katika hatua nyingine, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimewataka wananchi na wanachama wa chama hicho wajitokeze kujiandikisha kwenye daftari la wakazi na kujitokeza katika kupiga kura katika Serikali za Mitaa ili kurahisisha kazi ya kukiondoa madarakazi chama tawala kwenye uchaguzi mkuu hapo mwakani.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Njombe mkoani Njombe Naibu Katibu mkuu wa chama hicho Zanzibar amesema msingi wa serikali unaanzia ngazi ya chini hivyo wananchi kwa ujumla wasifikirie kazi ya kukiondoa chama tawala ni katika Uchaguzi mkuu pekee.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho bara Mh. John Mnyika amewataka wananchi kutopuuza nafasi za Uongozi katika mitaa na vijiji kwa kuwa hao ndio wasimamizi wakuu wa maendeleo katika maeneo yao.