Jumatatu , 27th Oct , 2014

Rais Jakaya Kikwete amekuwa kiongozi wa kwanza duniani kupokewa rasmi na pikipiki za polisi na kuongozwa na pikipiki hizo kwa muda wote wa ziara katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, nchini China.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesababisha mageuzi makubwa kwa namna Jamhuri ya Watu wa China inavyowapokea viongozi wageni kutoka nje kwa kuwa kiongozi wa kwanza duniani kupokewa rasmi na pikipiki za polisi na kuongozwa na pikipiki hizo kwa muda wote wa ziara katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Rais Kikwete ambaye aliwasili nchini China Jumanne iliyopita, Oktoba 21, 2014, kuanza ziara rasmi ya siku sita nchini humo, amekuwa kiongozi wa kwanza wa nje kupokelewa na msafara wa pikipiki tokea Januari Mosi, mwaka 2004, miaka 10 iliyopita wakati China ilipofuta utaratibu wa misafara ya viongozi kusindikizwa na pikipiki za polisi.

Rais Kikwete na msafara wake alipokewa na msafara wa pikipiki wa polisi mara baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Beijing hadi kwenye Nyumba ya Kufikia Wageni wa Serikali ya Diaoyutai, katikati ya Jiji la Beijing na utaratibu huo kuendelea kuongoza msafara wake kwa siku zote alipokuwa China.

Taarifa ya habari iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya China na kukaririwa na Shirika la Habari la nchi hiyo la Xinhua haikutoa sababu zozote za mabadiliko ya sera hiyo.

Katika nchi karibu zote duniani, utaratibu wa viongozi wa nchi mbali mbali kupokelewa kwa misafara ya pikipiki ni protokali ya juu kabisa ambayo pia huongeza usalama wa kiongozi na ni utaratibu wa kawaida katika nchi nyingi duniani.

Tokea kuasisiwa kwake mwaka 1949, Jamhuri ya Watu wa China ilikuwa na utaratibu wa pikipiki za polisi kuongoza misafara ya viongozi lakini utaratibu huo ulisimamishwa Januari Mosi, mwaka 2004, kwa sababu ambazo hazijapata kuelezwa.

Baada ya kuweka historia hiyo ya kuwa kiongozi wa kwanza wa nchi ya kigeni kupokelewa na msafara wake kuongozwa na msururu wa pikipiki nane, Rais Kikwete anatarajiwa kuondoka China leo, Jumatatu, Oktoba 27, 2014, baada ya kuwa amemaliza ziara yake rasmi.
Rais Kikwete anatarajiwa kuanza ziara rasmi ya siku mbili katika Vietnam kwa mwaliko wa Mheshimiwa Truong Tan Sang, Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam ambako miogoni mwa mambo mengine nchi hizo mbili zitaadhmisha miaka 50 tokea kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya nchi hizo mbili.

Miongoni mwa shughuli zake kubwa, Rais Kikwete atakutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha Vietnam, Mheshimiwa Nguyen Phu Trong na Mwenyekiti wa Bunge la Vietnam, Mheshimiwa Nguyen Sinh Hung.

Aidha, Mheshimiwa Rais atatembelea taasisi mbalimbali zenye uhusiano wa kiuchumi na Tanzania ikiwemo Kampuni ya Viettel inayotaka kuwekeza katika mawasiliano ya simu za maeneo ya vijijini katika Tanzania kwa bei nafuu zaidi.