
Akizungumza na EATV kwa njia ya simu Dkt Baraka Mwasankumbo Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Ikuti amewataja waliofariki kuwa ni Tumsifu Hosiana Mbughi(14)jinsi ya kike mwanafunzi wa kidato cha pili Sekondari ya Ikuti na Bryan Ngairo(11) jinsi ya kiume mwanafunzi wa darasa la sita Shule ya Msingi Kinyika.
Waliojeruhiwa ni pamoja na Hubiri Hosiana Mbughi (5),Tumepewa Hosiana Mbughi (3) na Neema Lusajo Kalinga(11) na baada ya kupatiwa matibabu hali zao zinaendelea vema wameruhusiwa kurejea mwakwao.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kezaria Simeon Kabula Seme amesema alipata taarifa za tukio hilo majira ya saa 8:00 mchana ndipo alipofika eneo la tukio ambapo majirani waliwawahisha Kituo cha Afya Ikuti na kuthibitika vifo vya wanafunzi wawili na majeruhi watatu na kwamba walikuwa kwenye masomo ya ziada (tuition) ndipo wakakutwa na ajali.
Diwani wa Kata ya Ikuti Charles Kalinga amefika msibani kwa kwa ajili ya kuwafariji wafiwa na kuwaona majeruhi Kituo cha Afya Ikuti.
Hata hivyo ameishukuru ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe na ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa kufika mapema eneo la tukio wakati huo akiomba Serikali kufunga vyombo vya kudhibiti radi kutokana na kuwepo kwa matukio ya mara kwa mara katika Kata yake.
"Hivi karibuni Afisa Utumishi alinusurika kifo alipokuwa akitekeleza majukumu yake ofisi ya Mtendaji Kata ilhali mtu mmoja alifariki baada ya kupigwa na radi miaka miwili iliyopita"alisema Kalinga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Benjamin Kuzaga kwa sasa yupo nje ya Mkoa hivyo Kaimu Kamanda amesema mpaka awe kwenye nafasi nzuri ya kulizungumzia suala hilo.