Alhamisi , 28th Aug , 2025

Hakuna viongozi wa nchi za Magharibi watakaokuwa miongoni mwa wakuu 26 wa nchi na serikali za kigeni watakaohudhuria gwaride hilo wiki ijayo isipokuwa Robert Fico, waziri mkuu wa Slovakia, nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya, kulingana na wizara ya mambo ya nje ya China.

Rais wa Urusi Vladimir Putin na Kim Jong Un wa Korea Kaskazini ni miongoni mwa viongozi watakaohudhuria gwaride la kijeshi mjini Beijing, ikiwa ni mara ya kwanza kuonekana hadharani kwa viongozi hao wawili pamoja na Rais Xi Jinping.

Hakuna viongozi wa nchi za Magharibi watakaokuwa miongoni mwa wakuu 26 wa nchi na serikali za kigeni watakaohudhuria gwaride hilo wiki ijayo isipokuwa Robert Fico, waziri mkuu wa Slovakia, nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya, kulingana na wizara ya mambo ya nje ya China katika taarifa yake ya leo Alhamisi Agosti 28.

Kutokana na hali ya kuongezeka kwa nguvu za kijeshi za China wakati wa gwaride la Siku ya Ushindi mnamo Septemba 3, viongozi hao watatu wataonyesha mshikamano mkubwa sio tu kati ya China na Ulimwengu wa Kusini, lakini pia kwa Urusi na Korea Kaskazini ambazo zinakabiliwa na vikwazo vya kiuchumi kimataifa.

Urusi, ambayo Beijing inaihesabu kama mshirika wa kimkakati, imewekewa  vingi zaidi na Magharibi baada ya uvamizi wake wa Ukraine mnamo 2022, huku ikitajwa kuwa uchumi wake ukielekea kudorora kutokana na vita hivyo. Putin, anayesakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, alisafiri mara ya mwisho China mnamo 2024 huku hii ikiwa mara yake ya kwanza tangu kuanza kwa mwaka 2025.

Korea Kaskazini, ambayo ni mshirika rasmi wa China, imekuwa chini ya vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tangu 2006 kutokana na utengenezaji wake wa silaha za nyuklia na makombora ya balestiki. Kim alitembelea China mara ya mwisho Januari 2019.

Watakaohudhuria gwaride la kuashiria kujisalimisha rasmi kwa Japan wakati wa Vita vya Pili vya Dunia ni pamoja na Rais wa Belarus Aleksandr Lukashenko, Rais wa Iran Masoud Pezashkian, Rais wa Indonesia Prabowo Subianto na Spika wa Bunge la Kitaifa la Korea Kusini Woo Won-shik, alisema Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa China Hong Lei katika mkutano na waandishi wa habari. Rais wa Serbia Aleksandar Vucic pia atahudhuria gwaride hilo.

Umoja wa Mataifa utawakilishwa na Naibu Katibu Mkuu Li Junhua, ambaye hapo awali alihudumu katika nyadhifa mbalimbali katika wizara ya mambo ya nje ya China, ikiwa ni pamoja na kuwa balozi wa China nchini Italia, San Marino na Myanmar.