Ijumaa , 10th Nov , 2023

Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza linamshikilia Joseph Hezron (54), mkazi wa Bukara wilayani Sengerema kwa kuchoma moto nyumba ya mpenzi wake aitwaye Lucy James, kisha kujaribu kujiua kwa kujichoma kisu shingoni huku chanzo kikitajwa kuwa ni wivu wa mapenzi.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza SACP Wilbroad Mutafungwa

Tukio hilo limetokea Novemba 9, 2023 katika mtaa wa Bukara baada ya Joseph kumtuhumu mpenzi wake huyo kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanaume mwingine aitwaye Jelemia Kamambi, ndipo alichoma nyumba hiyo na kupelekea hasara.

Uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi umebaini kuwa mwanaume ambaye Joseph alikuwa anamtuhumu hakuwa mpenzi wa mwanamke huyo (Lucy Hezron) bali alikuwa kaka yake, hivyo  kuwataka wanaume kuacha wivu wa mapenzi uliopitiliza.

Hata hivyo, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza SACP Wilbroad Mutafungwa, amesema walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo aliyekuwa amejificha porini baada ya kutenda uhalifu huo na anaendelea na matibabu katika hospitali ya wilaya ya Sengerema baada ya kujijeruhi kwa kujaribu kujiua, kisha atafikishwa mahakamani uchunguzi utakapokamilika.