Jumatatu , 13th Jun , 2022

Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya, limetangaza msako kwa wahusika wote wa mauaji ya Padre wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mbeya, Michael Samson (63), Raia wa Malawi, kilichotokea  kwenye mazingira ya kutatanisha baada ya kutoweka na mwili wake kupatikana maeneo ya Sabasaba kando ya mto Meta.

Kushoto ni Padre Michael Samson, na kulia ni RPC Mbeya Ulrich Matei

Kwa mujibu wa Taarifa ya Kamanda wa Jeshi la Polisi, Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei, amesema chanzo cha kifo cha Padre Samson ambaye alikuwa akihudumu katika Shirika la Missionaries of African (WHITE FATHER) kinachunguzwa.

Akielezea tukio hilo Kamanda Matei amesema Juni 10, mwaka huu Padre huyo aliwaaga wenzake kuwa anakwenda kufanya mazoezi ya kutembea na hakurudi tena hadi Juni 11 mwili wake ulipokutwa umetenganishwa kichwa na kiwiliwili na kisha kuviringishwa kwenye duveti na blanketi na kutupwa kwenye mto huo.

Kamanda Matei amesema ni kilomita mbili kutoka maeneo ya Parokia (Youth Center) mahali ambapo wanaishi mapadre wa shirika la  White Father hadi eneo ambalo mwili wake umekutwa.