Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Waziri Mkuu amepokea msaada huo kwenye shule mpya ya msingi Kakuni ambayo bado inaendelea kujengwa kwenye kijiji cha Kibaoni.
Akizungumza katika hafla hiyo fupi mara baada ya kupokea msaada huo, Waziri Mkuu Pinda aliishukuru kampuni ya General Booksellers Ltd ya kutoka Dar es Salaam kwa msaada huo ambao alisema utachangia kwa kiasi kikubwa kuitimiza ndoto yake aliyokuwa nayo ya kuisaidia jamii iliyomsomesha.
“Wazo la ujenzi wa shule mpya ya msingi Kibaoni lilitokana na ukweli kwamba nilisoma na kumaliza kwenye shule hii ya Kakuni. Nikiwa ni mtumishi wa Serikali, ni Mbunge na sasa hivi ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nilijiuliza hivi shule hii ninaweza kuiacha hivi hivi?”
“Nilijiuliza sana ni jambo gani ambalo naweza kulifanya la kusaidia wanakijiji wenzangu na kata nzima ya Kibaoni kama shukrani kwa kunilea na kunifikisha hapa nilipo. Ndipo wazo la kujenga shule niliyosoma likazaliwa kama mwaka mmoja na nusu uliopita,” alisema Waziri Mkuu wakati akiwahutubia wazazi, walimu na wanafunzi.
Mapema, akiwasilisha msaada huo, mwakilishi wa kampuni ya General Booksellers Ltd, Bw. Joachim Masaburi alisema wameamua kuchangia vitabu hivyo kwa kutambua umuhimu wa elimu kwa watoto lakini pia wanatambua juhudi za Serikali za kutoa elimu bora.
Akitoa mchanganuo wa vitabu hivyo, Bw. Masaburi alisema: “Kuna vitabu 600 kwa ajili ya shule ya awali ambavyo kati yake 300 ni vya ngazi ya chini (nursery) na vitabu vingine 300 ni vya ngazi ya juu (pre-school). Vyote ni vya hisabati, Kiingereza na sayansi”.
“Kwa shule ya msingi wao tunawapatia kivunge cha kufundishia mfumo wa mwili wa binadamu kama sehemu ya masomo ya sayansi, hiki kina thamani ya sh. 550,000/-,” alisema.
Pia kampuni hiyo ilitoa msaada wa vitabu vingine 295 vya Baiolojia, Fizikia, Uraia, Kiswahili kwa ajili ya shule ya sekondari ya Mizengo Pinda iliyoko kijijini hapo.
Hadi sasa majengo yaliyokamilika kwenye shule hiyo ni madarasa 14, jengo la utawala lenye ofisi za walimu na maktaba mbili (wanafunzi na walimu), jengo la TEHAMA la wanafunzi lenye darasa moja, ukumbi mdogo na ofisi za walimu na jengo moja la choo lenye matundu 48. Pia ujenzi wa nyumba sita za walimu uko kwenye hatua ya kuezeka. Nyumba hizo zinajengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). Ujenzi wa choo kingine chenye matundu 48 umeanza.
Waziri Mkuu aliwaomba wananchi wengine wamsaidie kutimiza ndoto yake kwani bado anakabiliwa na kazi ya kuweka umeme, maji, kujenga nyumba nane za walimu, bwalo na jiko, karakana nne za ufundi, ujenzi wa kituo cha walimu cha mafunzo ya muda mfupi na utunzaji taarifa (Resource Centre), viwanja vya michezo vya kisasa vinavyozingatia michezo yote, mfumo wa uvunaji maji ya mvua, mfumo wa maji safi na maji taka, nyumba mbili za walinzi na uzio wa shule.
Alitaja vitu vingine ambavyo bado vinahitaji kuchangiwa ni meza za walimu – za ofisini na darasani, viti vya walimu – vya ofisini na darasani, madawati ya shule ya msingi na ya awali, meza na viti vya maktaba zote mbili, meza na viti vya bwalo – shule ya msingi na shule ya awali.